Taasisi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imekanusha uvumi unaosambaa kuwa hukata viungo vya majeruhi wa ajali, hususan waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, bila kuwapatia matibabu stahiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dk. Mpoki Ulisubisya, ametoa ufafanuzi huo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha siku 100 za uongozi wake.
Amesema uvumi huo hauna ukweli, akibainisha kuwa kukata kiungo cha mgonjwa si jambo linalofanyika kiholela, bali ni hatua ya kitabibu inayochukuliwa pale tu inapobidi kuokoa maisha ya mhusika.
“Unakuta mtu anapata ajali na kupelekwa katika kituo kisicho na utaalamu huo. Akiwa huko majeraha yanazidi kuharibika, wakati mwingine vidole au mguu hubadilika rangi na kuwa mweusi kabisa. Anapofikishwa MOI, ili kumuokoa maisha, madaktari hulazimika kukata kiungo kilichoathirika. Hali hii ndiyo inaleta taswira kuwa tunakata viungo bila sababu, jambo ambalo si kweli,” amesema.
Amefafanua kuwa changamoto kubwa ni kuchelewa kwa wagonjwa kufikishwa katika hospitali yenye uwezo wa kutoa matibabu ya kibobezi mapema, jambo linalosababisha madhara makubwa zaidi.
MOI imesisitiza kuwa inaongozwa na misingi ya kitaalamu na kisheria katika utoaji wa huduma, na kwamba lengo kuu la madaktari wake ni kuokoa maisha na kuhifadhi viungo vya wagonjwa kadri inavyowezekana.
Chanzo; Nipashe