Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Wanafunzi 16 Wanusurika Ajalini Gari Likitumbukia Korongoni

Wanafunzi 16 wa Shule ya Msingi FM Foundation wamenusurika kifo baada ya gari aina ya Toyota Hiace lililokuwa limewabeba kutumbukia korongoni katika Mtaa wa Bonite, Kata ya Shirimatunda, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Tukio hilo limetokea leo Februari 11, 2026 majira ya saa 3:00 asubuhi, baada ya gari hilo kudaiwa kupata hitilafu ya mfumo wa uendeshaji (usukani), hali iliyosababisha dereva kushindwa kulimudu na kupoteza mwelekeo.

Akizungumza katika eneo la tukio, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Gadaffi Masod, amesema walipokea taarifa ya dharura kuhusu ajali hiyo na kufika haraka kwa ajili ya uokoaji.

“Tulipokea taarifa ya ajali iliyohusisha wanafunzi kuingia korongoni. Tulipofika tulikuta gari aina ya Hiace likiwa limetumbukia korongoni,” amesema Masod.

Ameeleza kuwa gari hilo lilikuwa limebeba wanafunzi 16 pamoja na dereva na kondakta. Katika operesheni ya uokoaji, wote waliokuwamo ndani ya gari hilo waliokolewa salama.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, wanafunzi wanne — wawili wa kiume na wawili wa kike — walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, kwa matibabu zaidi. Wanafunzi wengine 12 walitoka salama bila majeraha makubwa.

Amebainisha kuwa kati ya wanafunzi 16 waliokuwamo ndani ya gari hilo, 10 ni wa kike na sita wa kiume.

Masod amesema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu ya mfumo wa usukani (steering lock), iliyomfanya dereva kushindwa kulimudu gari na hivyo kutumbukia korongoni.

 

 

 

Chanzo; Nipashe

Kuhusiana na mada hii: