Kila inapofika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani waumini wa dini ya Kiislamu wanafunga kwa kujizuia kula na kunywa kuanzia Alfajiri (kuchomoza kwa jua) hadi Magharibi (kuzama kwa jua).
Kufunga saumu ni moja ya nguzo tano za Uislamu. Muislamu yeyote mwenye afya njema, akili timamu anatakiwa kushiriki katika ibada ya mfungo kwa kujizuia kula chakula chochote katika kinywa chake, kwa muda wote wa mchana kutwa.
Lakini awamu hii imekuwa tofauti kwakuwa Waislamu wanafunga Ramadhani wakati huo Wakristo nao wakifunga Kwaresma kwa wakati mmoja, jambo ambalo halijawahi kutokea kabla.
Visiwani Zanzibar, kula hadharani wakati wa mchana wa Ramadhan ni jambo ambalo limepigwa marufuku na mamlaka, na kwamba huwenda awamu hii hali hiyo itakuwa rahisi zaidi katika utekelezaji wake kwakuwa waumini wa madhehebu mbalimbali wako katika ibada hiyo ya mfungo.
Siku chache zilizopita mamlaka visiwani huko zilitoa taarifa ya kupiga marufuku migahawa kufunguliwa, watu kula hadharani pamoja na kutokupiga miziki mchana, agizo ambalo limesababisha migahawa ya chakula kufungwa wakati wote wa mchana na kufunguliwa baada ya muadhini wa Sala ya Magharibi.
Chanzo; Nipashe