Mfanyabiashara wa mazao Elia Juma Msabaha (27) ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam amekutwa ameuawa wilayani Makete Mkoa Njombe.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 1, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi la Polisi mkoani humo.
Amesema Agosti 28, 2025 mfanyabiashara huyo aliondoka Dar es Salaam na kuelekea wilayani Makete kwa ajili ya kununua mazao alipofika huko Agosti 29, 2025 inadaiwa aliuawa na mtu aliyefahamika kwa jina la Khalfan Mbilinyi kwa kumpiga na kitu chenye ncha butu kwenye paji la uso.
"Alimuua kisha kuchimba na kumfukia nyuma ya ghala lake ya kuhifadhia mazao," amedau Banga.
Amesema ndugu wa mfanyabiashara huyo walijaribu kufanya mawasiliano naye bila mafanikio na kufunga safari mpaka Wilaya Makete na kumtafuta bila ya mafanikio ya kumpata.
"Waliamua kufika kituo cha polisi wilayani Makete na kutoa taarifa ya kutoonekana kwa ndugu yao na jalada lilifunguliwa na uchunguzi ukaanza," amesema Banga.
Chanzo: Mwananchi