Siku ya uchaguzi haikuwa njema kwa Salum Mlyatangu, mkazi wa Gongo la Mboto mkoani Dar es Salaam baada ya kujeruhiwa na bomu hali iliyosababisha mwili wake kujeruhiwa maeneo ya tumboni, kwapani, na mkononi.
Kutokana na hali yake ya kimaisha Mlyatangu ameshindwa kuendelea na matibabu na hivyo ameomba wadau na serikali kujitokeza kumsaidia ili aweze kunusuru uhai wake.
Mlyatangu alifikwa na madhila hayo akiwa katika maeneo yake ya kazi ambako bomu lililorushwa na askari waliokuwa wanatuliza ghasia za waandamanaji lilimpata na kumuachia majeraha.
Akizungumza na Nipashe Digital dada yake, Hajira Sagamiko anasema kwa sasa hali yake ni mbaya na anahitaji msaada wa haraka.
“Tunahitaji msaada kama wanafamilia ili ndugu yetu aweze kupona, tunaomba pia hata walioguswa na tukio hili watusadie chochote kwa kuwa gharama za matibabu ni kubwa pekeyetu hatuwezi.
“Hali yake sio nzuri na anahitaji kufanyiwa x-ray hawezi hata kutembea vizuri ana maumivu makali sana, ameshonwa kwenye kwapa mkoni na tumboni,” amesema Hajira.
Chanzo; Nipashe