Jeshi la Polisi, Kamisheni ya Polisi Zanzibar, limekanusha vikali taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa limetoa tamko la kuzuia wananchi kula mchana katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, likieleza kuwa taarifa hizo si za kweli na hazijatolewa na Jeshi hilo.
Kupitia taarifa yake rasmi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo, imeeleza kuwa uvumi huo hauna msingi wowote na umelenga kupotosha umma, hivyo limewataka wananchi kupuuza taarifa hizo na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Aidha, Jeshi hilo limewasihi wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu pamoja na kuheshimu mila, desturi na sheria za nchi katika kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Jeshi la Polisi pia limekumbusha umuhimu wa kupata taarifa sahihi kupitia vyanzo rasmi vya Jeshi hilo na kuepuka kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho, ambazo zinaweza kusababisha taharuki au upotoshaji katika jamii.
Chanzo; Wasafi Media