Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amewasili jijini Geneva, nchini Uswisi, kushiriki Mkutano wa Ngazi ya Juu katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ulioanza Februari 23, 2026.
Katika mkutano huo Mhe. Homera anatarajia kuwasilisha taarifa rasmi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayofafanua hali ya haki za binadamu na hatua mbalimbali ambazo nchi imepiga katika eneo hilo.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Dkt. Homera ametembelea Ofisi za Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania zilizopo Geneva kwa ajili ya maandalizi ya mwisho.
Akiwa ofisini hapo, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkuu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, Balozi Dkt. Abdallah Possi, pamoja na Naibu Mwakilishi wa Kudumu, Balozi Dkt. Hoyce Temu, ili kuratibu agenda za nchi katika jukwaa hilo la kimataifa.
Ziara hii ina umuhimu wa kipekee katika kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa kupitia ushiriki hai kwenye majadiliano ya haki za binadamu duniani.
Kupitia mazungumzo hayo na wanadiplomasia wetu, Mhe. Waziri amesisitiza dhamira ya serikali katika kuendeleza misingi ya kisheria na utawala bora, huku akihakikisha kuwa mchango wa Tanzania katika Baraza la Haki za Binadamu unaleta tija kwa taifa na jumuiya ya kimataifa.
Chanzo; Itv