Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Bandari Kavu Kupunguza Msongamano Tunduma

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Ndg. Jabiri Makame amesema kuongezeka kwa ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam, kumeongeza kiwango cha mzigo unaopita katika lango la Tunduma kwa mwaka, kutoka tani milioni 5.4 mwaka 2022-23 hadi tani milioni 9.5 mwaka 2025 ambayo ni sawa na asilimia 75 ya Shehena unaosafirishwa kwenda nje ya Tanzania.

Hivyo, msongamano wa malori umeongezeka kwa kiwango kikubwa na kwamba, pamoja na miradi mingine ya kukabiliana na tatizo hili iliyopo, utekelezaji wa Mradi wa Bandari Kavu Tunduma utasaidia kuondoa msongamano kwa kiwango kikubwa na kurahisisha uvukaji wa Mpaka sambamba na kukuza biashara kati ya Tanzania na baadhi ya nchi za SADC, kwani mradi huu pia unahusisha ujenzi wa barabara ya mchepuko kuelekea moja kwa moja katika eneo la kuvuka mpaka badala ya malori kupita katikati ya Mji wa Tunduma. Mradi huu pia ni sehemu ya ahadi ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni zake mkoani Songwe mwaka 2025 na utatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi.

RC Makame ameyasema hayo katika Kikao cha Wadau wa Utekelezaji wa Mradi kilichoitishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na kuratibiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Wenye Ulemavu ndugu Dkt. Jim Yonazi ikiwa ni utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba aliyoyatoa katika ziara yake mkoani Songwe.

Kwa upande wake Dkt. Yonazi alieleza kwamba mradi huo unakwenda kubadilisha uchumi wa Tunduma, na Halmashauri isiutazame mradi huo kwa mtazamo mdogo bali uutazame kwa mtazamo mpana na kuona fursa zingine zitokanazo na Mradi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma Bi Mariam Chaurembo alieleza kupitia Mpango Kabambe Halmashauri ilitenga eneo la ekari 1800 kwa ajili mradi huo na tayari Mwekezaji amelipa fidia Bil. 8 na eneo lenye ukubwa wa ekari 1,671.2 limeshalipwa na kutolewa hati.

Mradi huo utatekelezwa na Kampuni ya TAZACO na Kampuni ya Jiayou International Logistics ya nchini China.

 

 

 

Chanzo; Itv

Kuhusiana na mada hii: