Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha kutokea kwa tukio la uhalifu wa kutumia silaha ambapo watu watatu wasiojulikana wakiwa na silaha za moto walimshambulia Yengo Mwapina mkazi wa momba na kisha kumyang’anya Fedha taslimu kiasi cha Shilingi milioni 54 ambazo alikuwa ametoka kuchukua Benki.
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe hii leo imeeleza kuwa tukio hilo limetokea jumatano februari 4, 2026 majira ya saa 4:00 asubuhi, katika eneo la kisimani Mtaa wa Unyamwanga, kanda ya Tunduma ambapo “ Yengo Mwapina Mkazi wa Sogea Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, alishambuliwa na watu watatu wasiojulikana akiwa njiani akitoka Benki.”
“Washambuliaji hao walimfyatulia risasi na kumsababishia jeraha kiunoni upande wa kushoto na kumnyang'anya fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni Hamsini na nne (54,000,000) za Kitanzania, Muhanga alikimbizwa katika Kituo cha Afya Tunduma ambapo alipatiwa matibabu ya awali na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa ajili ya matibabu zaidi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea na uchunguzi wa kina sambamba na msako mkali ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafikisha Mahakamani kwa hatua zaidi.” Imeeleza taarifa ya Polisi mkoa wa Songwe.
Chanzo; Millard Ayo