Hatimaye mwili wa mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Abdilah Mussa maarufu kama ‘Banjoo’ (54), umezikwa huku familia yake ikiomba Serikali kusaka watuhumiwa waliompora uhai wake kinyume cha sheria.
Mwili wa Banjoo umezikwa jioni ya leo, Februari 20, 2026, katika makaburi ya familia yaliyopo eneo la Moivo, mkoani Arusha.
Marehemu, ambaye alikuwa mkazi wa Sanawari jijini Arusha, anadaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana Februari 12, 2026, chini ya jengo la ghorofa 10 linalomilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, alipokuwa akitoka mazoezini (gym).
Baada ya tukio hilo, hakujulikana alipo hadi Februari 18, 2026, mwili wake ulipokutwa kando ya barabara katika eneo la Bereko, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Taarifa zinaeleza kuwa mwili huo ulikuwa na majeraha makubwa kichwani, mikono ikiwa imevunjwa na macho yakiwa yametobolewa.
Akizungumza wakati wa mazishi, mke wa marehemu, Jamilla Mohamed amesema familia imepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa, huku wakisikitishwa na hali ya mwili wake ulivyokutwa.
“Kiukweli mume wangu amedhulumiwa sana maisha yake. Hata kama alifanya kosa lolote, hakustahili kuuawa kwa mateso ya namna hii. Ilipaswa afikishwe kwenye vyombo vya usalama na kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema mjane huyo.
"Kikubwa hatuoni mwelekeo wa haki ya mume wangu kupatikana naomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie suala hili ili haki ya mume wangu iweze kupatikana, maana sisi kama familia hatuna cha kufanya," amesema.
Canzo; Mwananchi