Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka wizara zinazohusika na masuala ya ajira zisimamie kikamilifu utekelezaji wa sheria zinazotaka kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania zisifanywe na wageni isipokuwa zile zinazohitaji utaalamu ambao nchi inaupungufu.
Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya wenye nyumba kumpangisha raia mmoja wa kigeni na kumruhusu mpangaji huyo apangishe watu wengine ndani ya nyumba hiyo jambo ambalo ni hatari kwa usalama na pia halina tija kibiashara.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Jumatano, Januari 14, 2026 alipofungua Kikao cha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi. Agizo hilo linalenga kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la wageni kufanya kazi au biashara ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania na kuliwezesha Taifa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa ajira.
Amesema kuwa ni lazima wataalamu wa ndani wasimamie sheria ipasavyo na kama kuna maeneo yanayokwamisha wayabainishe na yafanyiwe marekebisho.
“Hatuwezi kuleta watu wanaokuja kufanya kazi ambazo Watazania wanaziweza.” “Watanzania tuwe na wivu na nchi yetu, mfano mtu anamkodishia nyumba mgeni kwa dola 5,000 kwa mwaka na kisha mgeni huyo anawaleta wenzake 60 na anawakodisha dola 500 hapo Mtanzania anapata hasara, hii si sawa hata kwa usalama.”.
Chanzo; Eatv