Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila @albert_john_chalamila amefika katika nyumba namba 59, makutano ya Mtaa wa Mkunguni na Bonde, kuingilia kati mgogoro wa mirathi unaomhusisha Bi Malaya, huku shauri hilo likiwa linaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo, RC Chalamila alisisitiza kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kujichukulia sheria mkononi, akionya kuwa hatua zozote za nguvu au uvamizi hazitavumiliwa.
Alieleza kuwa migogoro ya ardhi na nyumba inapaswa kushughulikiwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria hadi pale Mahakama itakapotoa uamuzi wa mwisho.
“Mtu hawezi kudai mali aliyokosa kujenga au kuishughulikia kisheria. Watoto na wajukuu wa marehemu ndio wanaostahili kushughulikia mali hiyo kwa manufaa yao, si mtu mwingine. Ni jukumu la Mahakama kuamua na kuhakikisha hukumu inatekelezwa,” alifafanua Chalamila.
Aidha, aliwataka wahusika wa mgogoro huo kuwa watulivu na kuheshimu mchakato wa kisheria unaoendelea, akiahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo katika eneo hilo.
Chanzo; Crown Media