Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Ruwa’ichi, amewaonya watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha kuacha kuchukua nafasi zilizotengwa mahususi kwa watoto wa familia maskini katika shule zinazohudumia wahitaji.
Akitoa mfano wa Shule ya Wasichana ya Makurunge iliyoko Bagamoyo mkoni Pwani iliyoanzishwa na Masista wa Mama Maria kutoka Korea na Japan, Askofu Ruwa’ichi amesema kumekuwepo na baadhi ya matajiri wanaotaka kupeleka watoto wao katika shule hiyo inayosimamia dhana ya kuwahudumia wanyonge, jambo alilolieleza kama “kufuru na unyang’anyi.”
“Nilisisitize, kwa sababu kuna watu wengine ambao wana fedha za kutupa lakini wao nao wanataka kujaribu watoto wao wakasome Makurunge, hiyo ni kufuru, huko ni kuiba na huko ni kujikita mahali ambako siyo staha ya matajiri. Fursa hii imekusudiwa kwa mabinti kutoka familia duni wasio na uwezo wa kugharamia elimu. Tuiache fursa hii iwanufaishe walengwa,” amesema.
Askofu Ruwa’ichi ameongeza kuwa shule hiyo kwa sasa inahudumia zaidi ya wasichana 1,000 kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, ambao wanasomeshwa na kulelewa bure bila ubaguzi wa kikabila au kijamii. Amesema pia mradi huo umeanzisha Boys Town kwa ajili ya wavulana kutoka familia maskini jijini Dodoma.
Ameyasema hayo leo Jumamosi, Septemba 27, 2025, wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, akishukuru kwa mchango mkubwa wa kuwaleta masista hao nchini.
Chanzo; Mwananchi