Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa tuhuma za wizi wa gari la kubebea wagongwa (Ambulance) la Hospitali ya Manispaa ya Musoma.
Taarifa ya tukio hilo ilitolewa na uongozi wa Hospitali ya Manispaa ya Musoma Oktoba 25, 2025 majira ya saa 02:00 usiku katika Kituo cha Polisi Musoma mkoani Mara.
Taarifa hiyo ilieleza kuibwa kwa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili STM 7830, ambalo liliibiwa katika eneo la maegesho ya Hospitali ya Manispaa ya Musoma.
Kufuatia kupokelewa kwa taarifa hizo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara lilianza mara moja uchunguzi na ufuatiliaji wa kina, hatua iliyowezesha kubaini namna gari hilo lilivyotolewa pamoja na eneo lilipokuwa limefichwa.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara lilifanikiwa kulikamata gari hilo likiwa katika hatua za mwisho za kubadilishwa muonekano, kutoka gari la kubeba wagonjwa (ambulance) na kuwa gari la kibiashara la kubeba watalii.
Taratibu za kisheria za kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani zinaendelea kukamilishwa.
Chanzo; Itv