Jeshi la Polisi nchini limeonya dhidi ya tabia ya baadhi ya watu kutumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kutengeneza, kuandika na kusambaza maandishi pamoja na picha mjongeo zenye lengo la kuhamasisha watu kufanya vitendo vya kihalifu vinavyokwenda kinyume na maadili, utamaduni wa Mtanzania na sheria za nchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo, Vitendo hivyo vya kihalifu vinavyo sukumwa na dhamira ovu, pamoja na kwamba ni kinyume cha Sheria za nchi, vimekuwa vikisababisha hofu na taharuki kwa wananchi wema walio wengi kuliko wao bila sababu zozote za msingi.
"Tabia hizo na vitendo hivyo, vinatakiwa kukemewa na kupigwa vita na mtu yeyote yule anaye tambua umuhimu na thamani ya Amani kwa maisha yake na familia yake."
Jeshi la Polisi limewahakikishia Watanzania kuwa, litaendelea kuwasaka na kuwakamata na kuwafikisha katika mamlaka nyingine za haki jinai kwa hatua za kisheria, kama ambavyo limeshafanya kwa waliokwisha kamatwa.
"Ambao bado wanaendelea na uhalifu huo na hawajafikiwa na mkono wa Sheria, wasijidanganye bali watambue kinachosubiriwa ni muda na ukamilishaji wa taratibu za kuwafikia wakati wowote kulingana na ushahidi, kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi." Imeeleza taarifa ya Jeshi la Polisi
Chanzo; Wasafi