Udahili hafifu katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, umeisukuma Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kuendesha mafunzo maalumu kwa maofisa udahili na mitihani.
Lengo likiwa ni kurekebisha dosari za mifumo ya usajili na tathmini ya wanafunzi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza kutolewa leo mkoani Shinyanga na yatahitimishwa kesho, yakilenga kuongeza ufanisi wa mifumo ya udahili na mitihani, sambamba na kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinaakisi hali halisi ya vyuo.
Akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa NACTVET, Meneja wa Uthamini na Utunuku wa Baraza hilo, Dk. Obeid Mahenya, amesema udahili hafifu umeonekana wazi kwenye kanzidata ya NACTVET, hali isiyoendana na idadi ya wanafunzi waliopo vyuoni.
“Udahili unaoonekana kwenye mfumo hauendani na idadi halisi ya wanafunzi, jambo linaloathiri moja kwa moja mipango ya elimu na mustakabali wa wanafunzi,” amesema Dk. Mahenya.
Amesema udahili hafifu pamoja na ucheleweshaji wa upakiaji wa matokeo ya mitihani, umekuwa ukisababisha wanafunzi kukosa mikopo ya elimu, kuchelewa kuendelea na masomo, kutopata vyeti kwa wakati na kukosa fursa za ajira.
Ametolea mfano kuwa hadi Januari 20 mwaka huu, kulikuwa na chuo kimoja kilichosajili wanafunzi wanne pekee kwenye mfumo wa NACTVET kwa mwaka wa masomo 2025/2026, hali aliyoitaja kuwa ni kiashiria cha upungufu katika usimamizi wa udahili.
Kutokana na hali hiyo, amesema NACTVET ililazimika kuongeza muda wa usajili wa wanafunzi hadi Januari 31 mwaka huu, ili kutoa fursa kwa vyuo vyote kukamilisha usajili katika kanzidata ya baraza.
Amesema, serikali inatambua mchango mkubwa wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la ndani na nje ya nchi, akibainisha kuwa sekta hiyo ni nguzo muhimu ya uchumi wa viwanda na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050.
Chanzo; Nipashe