Wagonjwa 11 kati ya 56 waliobainika kuwa na tatizo la tezi dume katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia teknolojia mpya ya mvuke wa maji.
Upasuaji huo wa kitaalamu, unaotumia muda wa dakika 15 hadi 20, umefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini katika hospitali hiyo, na unatajwa kuwa ni moja ya mafanikio makubwa katika sekta ya afya.
Akizungumzia mafanikio hayo leo Februari 10, 2026, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo, amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa madaktari bingwa wa hospitali hiyo pamoja na madaktari bingwa kutoka nchini India, ambao waliweka kambi ya siku sita kuanzia Januari 26 hadi 31 na kufanikisha upasuaji huo.
“Tulifanikiwa kuwaona wagonjwa 56 waliokuwa na changamoto ya tezi dume hapa hospitalini kwetu, na tuliweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 11 ambao kesho yake waliweza kuruhusiwa,” amesema Gabriel.
Amesema, “Moja ya sifa ya upasuaji huu wa njia ya mvuke ni kuwa na muda mfupi, na mgonjwa anakaa hospitalini kwa muda mfupi. Anaweza kufanyiwa leo na kutoka leo au kesho, inategemea mwili wake unavyokuwa baada ya kufanyiwa upasuaji.”
Chanzo; Mwananchi