Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, imeendesha mafunzo kwa wakaguzi kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza ili kuwajengea uelewa, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha jamii haiathiriki na matumizi holela ya dawa yanayosababisha usugu, pamoja na zile zenye asili ya kulevya.
Mafunzo hayo yamefanyika leo wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, yakilenga kufundisha wakaguzi angalau watatu katika kila halmashauri ili kuwaongezea ujuzi wanapotimiza majukumu yao.
Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Aggrey Muhabuki amesema wakaguzi hao wamefundishwa mbinu mbalimbali za kikaguzi, miiko, na maaidli ya ukaguzi, njia za ukaguzi, na sayansi ya utoaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa.
Vilevile, wameelimishwa kuhusu muongozo wa utunzaji sahihi wa dawa na vifaa tiba, na namna ya udhibiti usambazaji na utunzaji wa dawa na tiba zenye asili ya kulevya.
Chanzo; Nipashe