Hali ya huzuni imetawala kwa wakazi wa Mtaa wa Mabibo, Kata ya Mabibo, baada ya kukutwa kichanga kikiwa kimetupwa katika Mto Gide asubuhi ya leo Jumatatu, Januari 26, 2026.
Mashuhuda wanasema walipoamka asubuhi walihisi kitu si cha kawaida katika mto huo, baada ya kwenda kuangalia wakakuta kichanga hicho kikiwa kwenye kisado.
Akielezea tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa huo, Naseeb Mangushi amesema alipokea taarifa za kutupwa kwa kichanga hicho mapema leo, ndipo alipochukua hatua ya awali.
"Baada ya serikali ya mtaa kupokea taarifa nikapiga simu Polisi ambao walikuja na kukichukua kichanga hicho. Matukio haya ni nadra sana kutokea hapa. Natoa rai wenye tabia hii kuiacha kwani ni kuvunja sheria,” amesema.
Mmoja ya mashuhuda hao, Jamila Mohamed amesema alivyokuwa ndani alisikia kelele kuwa mtoto katupwa, ndipo akatoka na kanga kuja kumfunika.
Amesema baada ya tukio hilo, polisi walifika kupiga picha, kuchukua maelezo kisha kuchukua mwili huo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Chanzo; Mwananchi