Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewatoa hofu wafanyabiashara na wasafirishaji wa mafuta kuwa haijafunga Bandari ya Bagamoyo, bali changamoto iliyokuwepo imepatiwa ufumbuzi na shughuli zitaendelea kama kawaida.
Hatua hiyo imekuja baada ya shughuli za uingizaji wa mafuta katika bandari hiyo kusimama kwa takribani miezi mitatu kufuatia uwekaji wa utaratibu mpya wa ulipaji wa ushuru wa bidhaa.
Akizungumza wakati wa ziara yake bandarini hapo, Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Mahawa Masatu, amesema kwa niaba ya Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda, kuwa kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza na kushauri kuhusu changamoto hiyo imekamilisha kazi yake na kuandaa utaratibu mpya wa ulipaji kodi utakaoanza kutumika rasmi Machi Mosi.
Amesisitiza kuwa bandari haikufungwa na kwamba kusimama kwa shughuli kulitokana na sintofahamu ya kikodi ambayo sasa imetatuliwa, akiwataka wafanyabiashara kuwa watulivu na kurejea katika shughuli zao.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema wafanyabiashara walisimamisha shughuli wakilalamikia masuala ya kodi, na kwamba majibu yaliyotolewa na TRA yameleta faraja na yatawawezesha kurejea kazini.
Ameeleza kuwa biashara ya mafuta katika Bandari ya Bagamoyo ni kubwa na kusimama kwake kumeathiri vijana wengi, akibainisha kuwa takribani vijana 400 walikosa ajira za muda kutokana na hali hiyo.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mafuta bandarini hapo, Shabani Hamsini, amesema kusimama kwa shughuli hizo kuliathiri uchumi wao na kufanya maisha kuwa magumu, huku Diwani wa Kata ya Dunda, Amir Mpwimbwi, akisema kurejea kwa shughuli hizo kutachochea uchumi wa eneo hilo na kuongeza mapato ya kodi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, mfanyabiashara Saidi Abeid ameishukuru TRA kwa kusuluhisha changamoto hiyo, akisema kurejea kwa usafirishaji wa mafuta kutarejesha matumaini kwa wafanyabiashara na vijana waliokuwa wakitegemea sekta hiyo kwa kipato chao.
Chanzo' Nipashe