Mbunge wa Geita Joseph Kasheku Musukuma ameishauri serikali kuacha kuteua wenyeviti wa bodi watu waliostaafu bali wateuliwe vijana wenye maono mapya yatakayolisaidia taifa kupiga hatua.
Msukuma, amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia mjadala kuhusu mpango elekezi wa maendeleo wa muda mrefu 2026/27-2050/51, mpango wa nne wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano 2026/27-2030/31 na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2026/27.
“Wenyeviti wa bodi sasa wataingia kwa kushindana ni jambo zuri sana na mimi leo ni kama mara ya nne nazungumza hili, mwenyekiti wa bodi ndiyo mbeba maono sasa mara nyingi imekuwa kama cheo cha shukrani.
“Mtu anastaafu na miaka 70 kashindwa kufanya kazi vizuri akiwa kazini ameshakuwa mstaafu maisha yamempiga kule unamchagua tena unampa mwenyekiti wa bodi hana hata anachoweza na muda wake wa Mungu umeshapita miaka 70 anaenda pale kukaa tuu matokeo yake tunaanza kusumbuana,” amesema.
Chanzo; Nipashe