Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Radi Yaua Askari Akimfuata Mkewe Shamba

ASKARI wa Jeshi la Akiba katika Kijiji cha Kambeni, Kata ya Miamba, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Stephano Zawadi (43), amekufa papo hapo kwa kupigwa na radi wakati akienda shambani kumpokea mkewe zamu ya kulinda mahindi yasiliwe na tumbili.

Tukio hilo lilitokea juzi jioni wakati mvua iliyokuwa imeambatana na radi na upepo mkali ikinyesha katika eneo hilo.

Inadaiwa kuwa askari huyo, ambaye alikuwa ametoka kwenye ibada, alirejea nyumbani kabla ya kuondoka kwenda shambani na kukumbwa na mkasa huo.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Sadiki Mbonea, alithibitsha kutokea kwa tukio hilo.

“Ni kweli kulikuwa na mvua kidogo, lakini radi zilikuwa nyingi na zilileta madhara jioni majira ya saa 10 na dakika kadhaa. Kijana mmoja amefariki dunia wakati akienda shambani kumfuata mke wake. Ameungua kifuani na shingoni,” alisema Mbonea.

Alisema askari huyo wakati wa uhai wake alikuwa mzee wa Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kambeni na siku hiyo hiyo alikuwa mhubiri kanisani, akiwahimiza waumini kuimarisha maisha yao ya kiroho.

“Jana alikuwa anahubiri kuhusu umuhimu wa kujenga maisha yetu na Mungu, jambo ambalo limetusikitisha sana. Hili si tukio la kwanza, kwani miaka ya nyuma radi iliwahi kuua watu wawili katika kijiji hiki,” alisema.

Alisema eneo hilo limekuwa likikumbwa na mvua zinazoambatana na upepo mkali na radi na kwamba miaka miwili iliyopita, watoto wawili walikufa baada ya kuangukiwa na udongo wakati wa mvua.

Akizungumza kuhusu kifo hicho, hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Yusti Mapande, alisema kuwa: “Tumesikitishwa na kifo cha mwenzetu aliyepoteza maisha akiwa katika shughuli zake za kila siku za utafutaji. Alikuwa askari wa Jeshi la Akiba na pia mkulima. Hatuna la kusema zaidi ya kumshukuru Mungu na kumuombea apumzike kwa amani.”

 

 

Chanzo; Nipashe

Kuhusiana na mada hii: