Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu, amesema mipango ya maendeleo katika sekta ya utalii haipaswi kuchanganywa na hoja za kidini, akisisitiza kuwa hakuna udini kwenye fedha na kwamba miradi ya kimkakati inapaswa kutekelezwa kwa masilahi ya Taifa.
Zungu ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Februari 6, 2026, huku akitumia mfano wa historia ya Papa Leo, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, aliyewahi kuishi na kuhudumu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Morogoro, Songea, Dar es Salaam na Zanzibar.
Amesema Tanzania imepata bahati ya kipekee kuwa na historia hiyo, akipendekeza kujengwa kwa maeneo ya kumbukumbu yatakayovutia watalii wa ndani na nje ya nchi.
“Ukiweka maeneo ya kihistoria ya kidini shida iko wapi? Morogoro alikuwa anaishi nyumba gani, Songea alikuwa anasali kanisa gani, marafiki wa Papa Leo XIV walikuwa kina nani,” amehoji Zungu.
Ameitaka wizara inayohusika na utalii kuchangamkia fursa hiyo, akisema hoja za kudai udini hazina nafasi katika mipango ya kiuchumi.
Amesisitiza kuwa mipango ya Rais inahitaji utekelezaji na fedha, si maneno huku akionya kuwa kizazi cha sasa hakitaki kusubiri kwa kuwa, hakuna Taifa la kesho bila hatua za leo.
Chanzo; Mwananchi