Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Reuben Kwagilwa amewataka walimu wakuu wa shule za msingi nchini kushirikiana kwa karibu na Wazazi ili kuhakikisha Wanafunzi wanapata chakula ipasavyo wakiwa shuleni.
Kwagilwa ametoa maelekezo hayo baada ya kutembelea Shule ya Msingi Bagamoyo iliyopo Wilaya ya Korogwe Mkoa wa Tanga,akiwa njiani kukagua miradi itakayotembelewa na Waziri mkuu katika ziara inayoanza tarehe 13 mkoani Tanza na kukuta wanafunzi wakipata chakula cha mchana.
Mara baada ya kufika shuleni hapo amepata taarifa kuwa utaratibu huo umekuwa endelevu tangu mwaka 2018, ambapo wazazi wamekuwa wakijitolea kushirikiana na walimu kuwawezesha wanafunzi kupata chakula shuleni.
Akizungumza na wazazi aliowakuta shuleni hapo wakiwa katika kikao cha mkakati wa kuendelea kuwawezesha wanafunzi kupata chakula, Mhe. Kwagilwa amesema, “Utaratibu huu tuliouweka wa watoto kula shuleni ni utaratibu wa msingi sana, kwa hiyo niwapongeze wazazi wa wanafunzi wa shule hii ya Bagamoyo kwa kushirikiana na walimu bega kwa bega kuhakikisha watoto wetu wanakula hapa.”
“Utaratibu huu utatufanya tuongeze uwezo wa kufaulu kwa kuwa watoto watakuwa na muda mrefu wa kukaa na walimu, kutakuwa na utulivu na kupunguza utoro shuleni maana mtoto hatakaa anawaza njaa na tutawaimarisha watoto darasani.” Amesema Waziri Kwagilwa
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa rafiki kwa mwanafunzi na kuchochea ufaulu kupitia ushirikiano wa karibu kati ya walimu na wazazi.
Chanzo; Millard Ayo