Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi ametoa wito kwa viongozi na wote waliopo katika nafasi za uamuzi kuwajibika ipasavyo ili kurejesha imani na matumaini ya wananchi kwa Taifa lao.
Mwabukusi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Februari 2, 2026, wakati akiwasilisha salamu za TLS katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini 2026, yanayofanyika jijini Dodoma mgeni Rais akiwa Makamu wa Rais Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, akisisitiza kuwa uwajibikaji ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye haki, ukweli na uwazi.
Amesema TLS inatambua changamoto kubwa zilizoikumba nchi kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na kusisitiza kuwa njia pekee ya kusonga mbele ni kuhakikisha kila anayepaswa kuwajibika anafanya hivyo kwa masilahi mapana ya taifa.
“Ni lazima kuwe na hatua za uwajibikaji ili kurejesha imani na matumaini ya wananchi katika taifa lao. Ni rai yetu kwamba kila anayetakiwa kuwajibika awajibike,” amesema Mwabukusi.
Mwabukusi ameeleza kuwa kusamehe ni jambo jema pale mhusika anapokubali kuwajibika, kwani humpa nafasi ya pili, lakini kufumbia macho makosa ni sawa na kutojali mustakabali wa taifa.
Chanzo; Bongo 5