Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametajwa miongoni mwa wanawake 100 mashuhuri na wenye sifa ya juu wa asili ya Afrika kwa mwaka 2026.
Tuzo hiyo inayotolewa na Kongamano la Wanawake wa Afrika (Africa Women Summit), inatambua viongozi walioonesha uadilifu na mchango wa kipekee katika kuleta mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa barani Afrika na duniani kote.
Dkt. Gwajima ametambuliwa mahususi kwa juhudi zake za kuimarisha usawa wa kijinsia, ulinzi wa watoto, na uwezeshaji wa makundi maalum nchini Tanzania.
Akipokea heshima hiyo, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa uwezeshaji wanawake na kwa kumuamini kumpa nafasi ya kutumikia, akisisitiza kuwa utambuzi huo ni matokeo ya malezi bora na maono ya Rais katika kukuza uongozi wa wanawake.
Waziri Gwajima ameahidi kuendelea kuchochea "Kazi na Utu" akishirikiana na timu yake ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote, hususan wenye mahitaji maalum.
Heshima hii ya kimataifa kwa mwaka 2026 inalenga kuenzi wanawake wanaovunja vikwazo na kuhamasisha kizazi kijacho cha viongozi barani Afrika, huku Tanzania ikizidi kung'ara katika nyanja ya uongozi wa kidiplomasia na kijamii.
Chanzo; Itv