Mahakama Kuu ya Zanzibar imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na waliokuwa wagombea Uwakilishi wa ACT- Wazalendo kutoka majimbo 19 ya Unguja baada ya kukubaliana na pingamizi la wajibu maombi kwamba wakili aliyesaini kiapo kwenye maombi hayo hana leseni ya viapo.
Wagombea hao walipeleka ombi la zuio kwa hati ya dharura kufuatia tangazo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa umma likielezea nia ya kuteketeza nyaraka zote za uchaguzi wa mwaka 2025.
Ombi la zuio lilipelekwa mahakamani tayari kukiwa pia kuna ombi jingine la kugundua uwepo wa nyaraka mbalimbali na kupatiwa nakala hizo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya upande wa wajibu maombi (Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Uchaguzi Zanzibar) kabla ya kuanza kusikilizwa kuweka pingamizi kwamba wakili aliyesaini hati hizo licha ya kwamba ana sifa ya uwakili lakini hana leseni ya viapo, kwa hiyo hana sifa na kuomba Mahakama iyatupilie mbali.
ACT-Wazalendo imeendelea kukumbwa na mapigo ya kisheria baada ya Mahakama Kuu ya Zanzibar kutupilia mbali kesi hiyo. Awali, kesi 14 zilizokuwa zimewasilishwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge katika majimbo ya Pemba, zilitupiliwa mbali.
Chhanzo; Mwananchi