Utata umeibuka baada ya diwani wa Kata ya Nyamugali Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Majaliwa Abbas Hamis kufariki dunia huku chama chake cha ACT- Wazalendo kikitilia shaka kifo chake lakini polisi wakisema kimetokana na ajali ya Pikipiki.
Kupitia ukurasa rasmi wa Instagram, ACT Wazalendo wameandika;
“Jana tarehe 25.01.2026 tumemzika Diwani wetu wa Kata ya Nyamugali Marehemu Majaliwa Abasi Hamisi, ambaye amekutwa amekufa tarehe 24.01.2026 katika mazingira ya kutatanisha ikidaiwa kuwa ametapa ajali barabarani.
“Hata hivyo mwili wa marehemu ulivyokaguliwa na ndugu umekutwa hauna michubuko/majereha yoyote yanayotokana na ajali, koti alilovaa limekutwa pembeni ya mwili wake barabarani, laini za simu yake zimetolewa na kukutwa simu bila laini zake na shingoni akionekana akiwa na alama za kunyongwa.”
“ACT-Wazalendo Mkoa wa Kigoma tunalaani vikali mwenendo huu wa matukio ya mauaji yanayoratibiwa tukiamini kutokana na ushindani wa kisiasa na Vyama. Ndugu wa marehemu pamoja na Chama chetu tunalitaka Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma kufanya uchunguzi huru wa mauaji haya ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Kwa upande wao polisi wamesema;
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limeona picha mjongeo na barua ya Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha Majaliwa Abbas Hamis ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Nyamgali ikielezwa kuwa kifo hicho kina utata na hakikutokana na ajali hivyo Serikali ifanye uchunguzi wa kina zaidi.
“Taarifa zilizopo Polisi na zilizo kusanywa hadi sasa kutokana na uchunguzi ni kwamba Januari 23, 2026 majira ya saa Nne (4) usiku zilipokelewa taarifa kuwa katika eneo la Kijiji cha Songambele kuna ajali ya mtu aliyekuwa anaendesha Pikipiki amegongwa.
“Askari Polisi walifika katika eneo la tukio na kukuta kweli kuna mtu amegongwa na amefariki dunia na Pikipiki ikiwa pale ikiwa imeharibika vibaya kutokana na kugongwa na mahindi aliyokuwa amebeba yamemwagika na kusambaa barabarani.
“Taratibu zote za kiuchunguzi kwenye eneo la tukio zilifanyika na kukusanya vielelezo vinavyo husiana na ajali hiyo. "
Chanzo; Itv