Wanafunzi 33 wa udaktari wa binadamu waliohamishwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kutoka Chuo Kikuu cha Mwanza (MzU) kwenda Chuo Kikuu cha Katoliki cha Sayansi na Afya Shirikishi (CUHAS), wameiomba serikali kuingilia kati ili kupatikana ada zao Sh. Milioni 73 zilizozuiwa na chuo hicho.
Wanafunzi hao ni kati ya 300 wa shahada ya kwanza ya udaktari wa binadamu walioondolewa MzU na kupelekwa CUHAS kwa ahadi ya ada zao kuhamishiwa wanakopelekwa, lakini imekuwa kinyume chake na kusababisha wazuiwe kuendelea na masomo na kufanya mitihani.
Waliondolewa chuoni hapo Disemba 2, 2025 baada ya TCU kukifungia MzU kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu kwa mwaka wa masomo 2025/26, baada ya chuo hicho kubainika kudahili wanafunzi mara kumi zaidi ya idadi iliyoruhusiwa kisheria (60).
Hata hivyo, baada ya miezi takribani mitatu ya masomo baada ya uamuzi huo, wanafunzi hao wameanza kupata changamoto ikiwemo kuzuiwa na vyuo vilivyowapokea, kufanya mitihani na kuhudhuria masomo kutokana na ada zao kutohamishwa mpaka sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza Februari 25, 2026, Kiongozi wa wanafunzi 33 wa udaktari waliokumbwa na changamoto hiyo, Rachel Erick ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza shahada ya udaktari wa binadamu chuo cha CUHAS, amesema wamefuatilia ada zao kwa miezi mitatu sasa bila mafanikio.
“Tuliahidiwa kwamba ada zetu zitahamishwa kwenye vyuo husika tunavyosoma, sisi wanafunzi 33 tunadai jumla ya Sh. Milioni 73 ambazo tulikuwa tumezilipa huko Mwanza University, na hizo ada tuliambiwa kwamba zitahamishwa kuja chuoni Bugando lakini tumefuatilia bila mafanikio yoyote,” amesema Rachel.
Chanzo; Nipashe