Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuendeleza utu ndani ya Serikali, akisema ni wajibu wa wabunge kuhakikisha suala hilo linakuwa utamaduni katika utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali.
Akichangia hotuba ya Waziri wa Mipango bungeni leo, Februari 5, 2026, Nape amesema misingi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaweka wazi utu wa binadamu kama nguzo muhimu, hivyo unapaswa kuonekana moja kwa moja katika mipango na vitendo vya serikali kwa makundi yote ya jamii.
“Nape amesema: ‘Katika imani tatu za Chama cha Mapinduzi mojawapo ni utu wa binadamu, kwa hiyo haikuwa bahati mbaya na mimi nataka kukiomba chama changu kuanzia mwanzo hapa tunapoanza mipango ya utekelezaji wa dira hili suala la utu liwe wazi tulione moja kwa moja kwenye mipango ya Serikali tukienda kwenye Machinga tuone utu, tukienda kwa wakulima tuone utu, tukienda kwenye matendo ya vyombo vya dola tuone utu, tukimung'unya maneno CCM itaondoka jamani’.”
Kwa mujibu wa Nape, utekelezaji wa Dira ya Taifa na mipango ya maendeleo unapaswa kuakisi kwa vitendo vya utu kwa wananchi, ikiwemo kwa wafanyabiashara wadogo (Machinga), wakulima, na katika namna vyombo vya dola vinavyotekeleza majukumu yao.
Ameonya kuwa kukosekana kwa utu dna kuishia kumung’unya maneno kunaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa chama na Serikali. Hivyo, amewataka wabunge na viongozi wote kuhakikisha utu unakuwa kipimo kikuu katika uamuzi na utekelezaji wa sera za umma.
Chanzo; Mwananchi