Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii zikidai kuwa Godlove Materu hajulikani alipo baada ya kukamatwa na watu wasiojulikana.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Materu (45), mkazi wa Chapwa katika Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe, alikamatwa na Askari Polisi na siyo watu wasiojulikana.
Aidha, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa tuhuma za makosa ya jinai yanayomkabili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtuhumiwa anadaiwa kupanga na kutekeleza vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Tunduma na viunga vyake.
Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa uchunguzi wa kesi hiyo umekamilika na hatua nyingine za kisheria zinaendelea kufuatwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewataka wananchi kuendelea kupuuza taarifa zote zinazozagaa bila uthibitisho kutoka kwa mamlaka husika au vyanzo rasmi.
Chanzo; Global Publishers