Serikali imekuja na mkakati maalumu wa kazi za staha unaolenga kuwawezesha wafanyakazi wa ndani kupatiwa mikataba, sambamba na kupata stahiki zao za kisheria na fursa mbalimbali za kiuchumu.
Hatua hiyo imeenda sambamba na uzinduzi wa programu ya taifa ya kazi za staha awamu ya tatu ya mwaka 2025/2026 – 2029/2030 na mkakati wa kukuza kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani.
Akizungumza jana Mkoani Dodoma wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema progamu hiyo inalenga kuimarisha majadiliano ya kijamii na mshikamano baina ya serikali, waajiri, wafanyakazi na wadau mbalimbali.
Waziri Sangu amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayo rahisisha utekelezaji wa programu hiyo ili kukuza maendeleo kupitia kazi za staha.
“Tanzania ni taifa linalojali utu, haki, mshikamano hivyo kuwa na kazi za staha ni msingi wa maendeleo endelevu," amesema Sangu.
Pia, Waziri Sangu amelishkuru Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa kuendelea kushirikiana na serikali katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kisera, programu, miongozo, mafunzo na miradi.
Chanzo; Nipashe