Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Manyara limebaini wizi wa umeme unaodaiwa kufanywa na mteja wao aitwaye John, mkazi wa Dareda, Wilaya ya Babati, wakati wa ukaguzi unaoendelea kufanywa na shirika hilo kwenye miundombinu yake.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Maisha Mchuruza, mkaguzi wa mita wa TANESCO, amesema walibaini kuwa matumizi ya umeme hayakuonekana kwenye mita ya mteja huyo kwa sababu alikuwa anautumia kabla haujaingia kwenye mita.
Hali hiyo imesababisha serikali na TANESCO kupoteza mapato.
“Baada ya kubaini wizi huo, tulichukua hatua za kumsitishia huduma ya umeme mara moja, mteja atalazimika kulipia gharama za umeme alioutumia bila kuonwa na mita pamoja na kulipa faini stahiki,” alisema Mchuruza.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa TANESCO mkoa wa Manyara, Samwel Mandari, alisema oparesheni ya kukagua na kudhibiti wizi wa umeme inaendelea nchi nzima na mkoa wa Manyara hauko nyuma.
“Tutapita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kuhakikisha kila mteja anatumia umeme kwa usahihi.
Tunakemea tabia hizi za kuiba umeme na tunawaonya wanaofikiria kufanya hivyo kuacha mara moja,” alisema Mandari.
Aidha, inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo, ambaye ni mfanyabiashara wa samani, alitoroka pamoja na mafundi wake baada ya kufika kwa maofisa wa TANESCO, na kumuacha mkewe na kijana mmoja kiwandani ambao walidai hawana taarifa yoyote kuhusu wizi huo.
Michael Burra, mmoja wa waliokutwa kiwandani, amesema pindi kunapotokea hitilafu, wamekuwa wakiwaita mafundi wa TANESCO wa kituo cha Dareda, na hawajawahi kufahamu kama kulikuwa na njia zisizo halali za kutumia umeme.
Cc Bongo 5