Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam iliyoketi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu kunyongwa hadi kufa Mama na Mtoto wake wa kiume baada ya kukutwa na hatia ya kumuua Mtu aitwae Beatrice Magombola ambaye ni Mtoto wa aliyekuwa Mume wa Mama huyo.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu aliyepewa Mamlaka, Mary Mrio ambapo aliwataja waliohukumiwa kuwa ni Sophia Mwenda na Alphonce Magombola (Mtoto) ambapo walitenda mauaji hayo kwa kutumia kisu tarehe 1 Disemba 2020 maeneo ya Kijichi, Temeke Jijini Dar es salaam.
Awali Hakimu Mrio alisema ushahidi uliotumika kuwatia hatiani Washtakiwa ni wa kimazingira ambapo Jamhuri ilionesha kwamba mwili wa marehemu uliokotwa eneo la Zinga Wilaya ya Bagamoyo ambapo ulichunguzwa na ukazikwa na Halmashauri ya Bagamoyo ambapo katika mahojiano Washtakiwa walikiri kutenda kosa hilo.
Imeelezwa kuwa Baba wa Beatrice alifunga ndoa na Mama huyu na baada ya kutengana Mama huyu aligushi nyaraka na kuuza nyumba ya Baba Beatrice iliyopo Mbeya na baadae kugundulika kuwa wameiuza isivyo halali ambapo Shahidi pekee wa kusimamia hilo ni Beatrice ambaye naye hakusita kulichachamalia swala hilo na kusema atakwenda hadi Mahakamani kutoa ushahidi nyumba ya Baba yake irudishwe.
Mama huyu na Mtoto wake wa kiume baada ya kubaini kuwa Beatrice ( ambaye ni Mtoto wa Mama mwingine) atakuwa kikwazo, walikwenda mpaka nyumbani kwa Beatrice Kijichi Dar es salaam ambako baada ya mvutano Mama huyu inadaiwa alichukua kisu na kumchoma Beatrice na kufariki kisha wakauchukua mwili wake na kuufunga kwenye mkeka na kwenda kuutupa Mto zinga ambapo baadae upelelezi wawili hawa walikamatwa na leo wamepatikana na hatia ya mauaji hayo.
Chanzo; Millard Ayo