Baraza Kuu la Waislamu nchini Tanzania BAKWATA na taasisi za Kiislamu nchini humo, limelaani vitendo vya vurugu vilivyotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29 na baadaye.
Tamko la BAKWATA, ambalo lilisomwa kwa vyombo vya habari na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa na Imam Mkuu wa Msikiti wa Maamur, Sheikh Issa Othman Issa mapema siku ya Alhamis, limelaani vikali vitendo vya uhalifu, vurugu, na uharibifu wa miundombinu na mali vilivyosababisha vifo vya watu wasio na hatia na ulemavu wa kudumu kwa wengine.
Aidha Baraza hilo limeiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliohusika kama vinara wa machafuko hayo. Wamesisitiza kuwa suluhu au maridhiano visitumike kama kificho cha kuwalinda wahalifu.
Tamko hilo limerejelea msimamo wa BAKWATA kuwa amani ni sharti la kupatikana kwa haki, na kwamba kudai haki ni halali lakini lazima kufanyike kwa njia zisizohatarisha utulivu wa taifa.
Chanzo; Dw