Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Mh. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, katika ziara yake rasmi ya kikazi kutembelea miradi mikubwa ya uwekezaji wa kimkakati ya Kampuni ya Sukari Kilombero (KSCL) yenye thamani ya zaidi ya shillingi bilioni 787 kwa Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda Kipya cha Sukari K4 na shilingi bilioni 200 kwa Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda cha Pombe ghafi (Distillery) cha K3.1.

Waziri aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Uchumi Tanzania (TISEZA), Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, pamoja na wawakilishi wengine waandamizi wa serikali.
Ziara ya Waziri ni sehemu ya ziara yake ya Mkoa wa Morogoro kukagua miradi ya uwekezaji ya kimkakati iliyopewa hadhi ya Special Strategic Investment Status na Strategic Investment Status. Mradi wa Kiwanda Kipya cha Kilombero 4 uliidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Uwekezaji (NISC) na kupatiwa Cheti cha Uwekezaji (COI) kutoka TISEZA.
Mradi huu wa upanuzi una thamani ya takribani Tsh 787 bilioni, huku Tsh 200 bilioni zikiwa ni kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha K3.1 Distillery, miradi ambayo inatekelezwa katika maeneo ya Kilombero na Kilosa. Kiwanda hicho cha sukari kinatarajiwa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 271,000 kwa msimu ifikapo mwaka 2030/31 kitakapofikia uwezo wa juu wa uzalishaji.

Wakati wa ziara yake kiwandani, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mh. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, alisifu kiwango cha uwekezaji huo na kueleza kuwa ni wa kipekee na miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa sukari kujengwa katika kipindi cha miaka 40 katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, na kwamba nchi inapaswa kujivunia.
Waziri Mkumbo alisema:“Uwekezaji huu ni miongoni mwa miradi iliyopata Cheti cha Uwekezaji (COI) kutoka TISEZA chini ya hadhi ya Special Strategic Investment Status. Nimefika kuona kwa macho hali halisi ukilinganisha na maandiko ya uwekezaji. Najivunia sana kuona hatua iliyofikiwa. Hongera kwa Kilombero Sugar kwa mradi huu mkubwa na wa kihistoria wa Kiwanda Kipya cha Sukari K4.”
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Kilombero Sugar, Bw. Guy Williams, alisema kuwa kampuni imetumia miaka mitano kuandaa na kutekeleza Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda cha Sukari K4, wenye lengo la kuiwezesha Tanzania kufikia kujitosheleza kwa sukari. Aliongeza kuwa kiwanda kipya kinatarajiwa kudumisha uzalishaji mara mbili hadi kufikia tani 271,000 ifikapo msimu wa 2030/2031.

Bw. Williams alisema: “Tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa serikali katika safari hii ya ujenzi wa mradi huu, na tunaendelea kutarajia kuimarisha ushirikiano huo zaidi.”
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Gilead Teri, alisifu uwekezaji huo na kueleza kuwa ni matokeo ya msukumo wa serikali kupitia hadhi ya Special Strategic Investment katika kuvutia uwekezaji mkubwa nchini. Alisema:“Tunawahamasisha wawekezaji wengine wa kimkakati kufuata njia kama ile iliyochukuliwa na Kilombero Sugar.”
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Prof. Kenneth Bengesi, alikiri umuhimu wa uwekezaji huo na kueleza kuwa utaleta mageuzi katika sekta ya sukari nchini. Alisema kuwa Kilombero Sugar pekee yake itachangia takribani asilimia 40 ya sukari yote inayozalishwa nchini. Aidha, Bodi ya Sukari itaendelea kushirikiana na wazalishaji kuhakikisha Tanzania inafikia kujitosheleza kwa sukari.
Mradi wa Upanuzi wa Kiwanda cha Sukari K4 unahusisha ujenzi wa kiwanda kipya chenye uwezo wa 420 TCH, ambacho kitaongeza uzalishaji wa sukari kwa tani 144,000—zaidi ya mara mbili ya uzalishaji wa sasa—na kufikia tani 271,000 kwa mwaka ifikapo 2030/31. Pia unatarajiwa kuongeza kiasi cha miwa kutoka kwa wakulima wa Bonde la Kilombero kutoka tani 600,000 hadi 1,500,000 kwa msimu—takribani mara tatu ya kiwango cha sasa.
Mradi huu unakwenda sambamba na dira ya Tanzania ya kufikia kujitosheleza kwa sukari na kuwa muuzaji wa sukari kwenye masoko ya nje.