Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amepata uungaji mkono mkubwa kutoka kwa viongozi wa mataifa mbalimbali pamoja na United Nations kufuatia ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Balozi Kombo amesema viongozi hao wamempongeza Rais Samia kwa ujasiri wake wa kurejesha amani nchini licha ya “mawimbi” ya machafuko yaliyochochewa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Ameeleza kuwa katika mikutano ya faragha iliyofanyika kando ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa African Union (AU) nchini Ethiopia, Rais Samia alikutana na viongozi wenye ushawishi mkubwa akiwemo Rais wa Angola na Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa AU, João Lourenço, pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Balozi Kombo amesema viongozi hao walimpongeza Rais Samia kwa ushindi mnono pamoja na namna alivyofanikiwa kudhibiti hali ya usalama baada ya uchaguzi.
Ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa imebaini kuwa maandamano na vurugu zilizojitokeza Tanzania ni sehemu ya “wimbi la kidunia” linalotumia mitandao ya kijamii kuvuruga mataifa kwa lengo la kugombea rasilimali.
Kwa mujibu wa Balozi Kombo, viongozi hao wameahidi kumuunga mkono Rais Samia kwa hali na mali, wakikumbuka mchango mkubwa wa Tanzania katika masuala ya ulinzi pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu, ikiwemo chakula wakati wa vipindi vya ukame.
Chanzo; Global Publishers