Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, George Joseph Kazi, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 98(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 2018.
Amefafanua kuwa sheria inaipa Tume mamlaka ya kuharibu nyaraka za uchaguzi baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria, hususan pale ambapo hakuna zuio lolote la mahakamani ndani ya siku 90 baada ya Uchaguzi Mkuu.
Zoezi hilo linafanyika kwa kuzingatia uwazi, usalama na taratibu zote za kisheria, kwa lengo la kulinda uadilifu wa mchakato wa uchaguzi pamoja na usalama wa taarifa zilizohifadhiwa. Zoezi hilo pia limeshuhudiwa na watendaji wakuu wa Tume, akiwemo Makamishna wa ZEC.
Tume imewahakikishia wananchi kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa kisheria na haina lengo jingine isipokuwa kutekeleza matakwa ya sheria.
Chanzo; Crown Media