Derick Mwangama (23), amejinyonga na kupoteza maisha mara baada ya kumuua mtoto wake wa miaka miwili, Deniva Derick kwa kutumia kamba ya manila huku uchunguzi wa awali ukionesha chanzo cha tukio hilo ni kuibuka kwa mgogoro baina ya baba na mama wa mtoto huyo ambao walikuwa wametengana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi Benjamin E.Kuzaga leo Novemba 21, 2025 amesema tukio hilo lilitokea Novemba 18, 2025 katika Kijiji cha Isaka, Kata ya Nkunga,Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Kabla ya tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo ambao wote ni marehemu, alikwenda nyumbani kwa mzazi kwenzie Violeth Edward (19) na kumchukua kwa nguvu mtoto huyo huku akiwa na jazba.
Baada ya kuondoka naye, baadaye mwili wa mtoto ulikutwa ukiwa umenyongwa na kisha kutekelezwa kando ya Mto Kiwira.
Amesema baba wa mtoto huyo ambaye ni marehemu baada ya kufanya mauaji hayo ya mwanaye, alijinyonga kwa kutumia kamba ya manila kwenye mti wa parachichi kando ya mwili wa mtoto wake.
Chanzo; Eatv