Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi,waliokuwa wakishambulia gari la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wakidai walichelewa kufika eneo la tukio wakati nyumba moja ikiteketea kwa moto.
Tukio hilo lilitokea leo Novemba 19,2025 majira ya saa 11 jioni katika eneo la maduka ya Manara wa Voda, baada ya moto kuzuka katika nyumba moja na kuteketeza mali mbalimbali, ingawa hakuna mtu aliyepoteza maisha.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema wananchi walikasirika baada ya kuona juhudi zao za kuuzima moto kwa kutumia ndoo za maji zikishindikana, huku wakidai kikosi cha Zimamoto kilichelewa kufika eneo la tukio.
Mmoja wa wananchi hao Solo Bundala, amesema hasira ndizo zilizosababisha baadhi yao kulipiga mawe gari la Zimamoto walipowasili kutokana na kuchelewa na kwamba wanaishi jirani na eneo la tukio.
“Wananchi wamejikuta wanachukua sheria mkononi kutokana na hasira za kuchelewa kwa kikosi cha Zimamoto, wakati vitu vingi tayari vilikuwa vimeteketea,” amesema Bundala.
Baby Mohamed, ambaye nyumba hiyo ni ya baba yake mdogo, amesema upande wa nyuma wanaishi kaya tano, huku mbele kukiwa na maduka matano ya wapangaji.
Mmoja wa wapangaji katika nyumba hiyo, Hidaya Selemani,amesema ilipofika majira ya saa 11 jioni, aliingia chumbani na kuwasha taa, ndipo akaona zinapiga short, muda kidogo akaona moto unalipuka chumba cha jirani, nakuamua kutimua mbio nje na watoto wake Sita.
Amesema, baada ya kutoka nje alianza kupiga kelele ya kuomba msaada, ndipo wananchi wakafika na kuanza kuuzima moto huo,lakini vitu vyake vyote vimeteketea na hakuna ambacho ameokoa.
Chanzo; Nipashe