Mwalimu amelazwa katika kituo cha afya cha Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro huku wanafunzi 11 wakijeruhiwa kutokana na kushambuliwa na Nyuki wakati wakiwa kwenye shughuli za usafi katika Shule ya Msingi Lukobe.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya Lukobe, Judith Ntanyinya, amesema baada ya kupatiwa matibabu wanafunzi hao 11 wameruhusiwa kurejea nyumbani, huku mwalimu wao akiendelea kupatiwa matibabu kituoni hapo.
“Wanafunzi wameruhusiwa lakini mwalimu bado amelazwa katika wodi ya wagonjwa kwa uangalizi zaidi kutokana na hali yake kutoridhisha,” amesema.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mohamed Mangu, amesema Nyuki hao walionekana kwa mara ya kwanza takribani siku nne zilizopita wakiwa wamekaa juu ya tanki la maji lililopo katika eneo la shule ambako uongozi wa shule ukijaribu kuziba njia waliyokuwa wakitumia kupita ili kuwafukuza juhudi ambazo hazikuzaa matunda.
Chanzo; Nipashe