Mkazi wa Dar es Salaam, Simon Bryson amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia matibabu ya mtoto wake Nilsa Simon kufuatia ombi lake kupitia mitandao ya kijamii mtoto wake asaidiwe matibabu .
Bw. Simon ametoa shukurani hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Taasisi ya MOI ambako mtoto wake anaendelea na matibabu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema Serikali imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kusaidia wananchi, hususani wenye changamoto za kiafya zinazohitaji matibabu ya gharama kubwa.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia imeweka kipaumbele katika afya za wananchi. Tumeendelea kupokea wagonjwa wengi wanaosaidiwa kupitia mifumo mbalimbali ya serikali, jambo linaloonesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia Watanzania,” amesema Dkt. Mpoki.
Naye Dkt. Hamis Shabani, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo wa MOI, amewataka wanawake kuchukua tahadhari mapema kabla ya ujauzito ili kuepuka matatizo ya kiafya kwa watoto wachanga.
Chanzo; Clouds Media