Serikali ya Angola imemtunuku hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, nishani maalumu ya heshima kwa kutambua mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi na kupatikana kwa uhuru wa nchi hiyo pamoja na amani ya kudumu.
Nishani hiyo, iliyotolewa katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Angola, imekabidhiwa jana, Januari 5, 2026, kwa mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, kama ishara ya shukrani na kumbukumbu ya mshikamano wa dhati wa Afrika wakati wa mapambano ya kuondokana na ukoloni.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingos de Almeida da Silva Coelho, amesema nchi yake inatambua mchango wa kipekee wa Nyerere katika kusaidia harakati za ukombozi wa Angola, akisisitiza kuwa bila msaada huo safari ya uhuru ingekuwa ngumu zaidi.
“Angola haitasahau mchango wa Mwalimu Nyerere. Tanzania ilikuwa nguzo muhimu katika mapambano yetu kwa kutoa hifadhi, mafunzo na msaada wa kimkakati kwa wapigania uhuru,” amesema Balozi Coelho.
Kwa niaba ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema utunuku wa nishani hiyo unaonesha namna mchango wa Mwalimu Nyerere ulivyovuka mipaka ya Tanzania na kuwa urithi wa bara zima la Afrika.
Akishukuru kwa niaba ya familia, Mama Maria Nyerere amesema anatambua na kuthamini heshima hiyo, akieleza kuwa mumewe alijitolea kwa dhati katika kuikomboa Afrika kwa imani kwamba uhuru wa taifa moja haukuwa na maana bila uhuru wa bara zima.
Chanzo; Mwananchi