Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga limewafuta kazi watumishi wanne wa halmashauri hiyo kwa tuhuma za utoro kazini hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.
Watumishi hao waliotimuliwa ni kutoka idara za afya, utawala, maliasili na kilimo, baada ya kubainika kutokuwapo katika vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu bila kutoa taarifa wala maelezo kwa waajiri wao kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu Gagi Lala, ametangaza uamuzi huo leo wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha Robo ya Pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, kinachohusisha kipindi cha Oktoba hadi Desemba, kilihusisha upokeaji na mjadala wa taarifa za maendeleo kutoka kata zote za halmashauri hiyo.
Lala amesema, uamuzi wa kuwafuta kazi watumishi hao umezingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma baada ya kubainika kuwa walikiuka maadili ya kazi kwa kuacha vituo vyao bila ruhusa.
“Hatutaendelea kuvumilia watumishi wasiowajibika, mtumishi anayeshindwa kuheshimu kazi yake anawakosesha wananchi haki ya kupata huduma stahiki" Ameongeza Lala.
Chanzo; Nipashe