Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Padri Kibiki Hakutekwa, Kanisa Latoa Ufafanuzi

Ufafanuzi umetolewa na kanisa Katoliki kufuatia kuenea kwa ripoti za kutekwa kwa Padri Jordan Kibiki siku chache zilizopita.

Akizungumza na wanahabari mkoani Iringa Septemba 30, 2025 Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Vincent Cosmas Mwagala, ameeleza kuwa Padri Jordan Kibiki hakutekwa kama ilivyoripotiwa awali, bali alikumbwa na hali ya unyongefu (depression) kutokana na hasara aliyopata kwenye biashara ya mtandaoni ya takribani Shilingi milioni 3.5 katika mtandao wa eBay.

Amefafanua kuwa kati ya fedha alizopoteza, Shilingi 500,000 alikuwa ameazima kwa Paroko na Shilingi milioni 1.5 kwa mhasibu wa jimbo, na kwamba kiasi kilichosalia kilitokana na fedha zake mwenyewe, hivyo hakukuwa na madeni makubwa ya kumfanya kujiingiza katika vitendo vya hatari.

Awali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kupitia Kamanda Allan Bukumbi lilieleza kuwa baada ya uchunguzi, Kibiki alikutwa Mbalizi mkoani Mbeya na hakuwa ametekwa kama alivyodai kupitia mtandao wa WhatsApp. Polisi walibainisha pia kuwa alitelekeza gari lake aina ya Toyota Harrier katika eneo la Sao Hill na kupanda basi kuelekea Mbeya.

Polisi waliongeza kuwa Padri Kibiki alitoa taarifa za uongo kuhusu kutekwa na kusafirishwa kwa gari aina ya Toyota Alphard lenye rangi nyeusi huku akidai mmoja wa watekaji alikuwa na bastola. Aidha, walieleza kuwa awali waliamini Kibiki alikuwa na madeni makubwa kutokana na mikopo aliyochukua kwa ajili ya biashara mtandaoni.

Jeshi la Polisi liliutumia tukio hilo kutoa onyo kali kwa viongozi wa dini na wananchi kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta taharuki na upotoshaji katika jamii. Askofu Mwagala amesema Kibiki tayari ameachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi limemfutia mashitaka yaliyokuwa yakimkabili. 

 

Chanzo: Eatv

Kuhusiana na mada hii: