Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia askari polisi mmoja kwa tuhuma za kumpiga risasi raia, huku likichunguza matukio mengine mawili ya vifo yaliyotokea Rorya mkoani Mara na Arusha.
Taarifa ya kukamatwa kwa askari huyo, imetolewa leo Alhamisi Januari 8, 2026 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kumpiga risasi na kusababishia kifo, Shaban Luluba mkazi wa Nyamwage, Rufiji mkoani Pwani.
Taarifa hiyo inaeleza, askari huyo wa Mkoa wa Kipolisi Rufiji, alifanya tukio hilo, alipokuwa katika ukamataji Januari 8, 2026.
“Uchunguzi unaendelea na endapo itabainika kuna uzembe au matumizi zaidi ya nguvu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi ya askari huyo,” amesema.
Chanzo; Mwananchi