Waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika wamesema kwamba uadilifu wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29 uliathiriwa, wakitaja matukio ya kujazwa kwa kura katika vituo kadhaa vya kupigia kura.
Ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa umoja huo ulisema hapo jana waangalizi wake walishuhudia wapiga kura wakipewa kura nyingi, huku baadhi wakiruhusiwa kupiga kura zao bila utambulisho wao kuthibitishwa katika orodha ya wapiga kura kwenye daftari la wapiga kura.
Ripoti ya awali kutoka kwa ujumbe wa Umoja wa Afrika inasema uchaguzi mkuu wa Tanzania wa 2025 haukuzingatia kanuni za Umoja wa Afrika, mifumo ya kanuni, na majukumu na viwango vingine vya kimataifa vya uchaguzi wa kidemokrasia.
Ujumbe huo ulisema waangalizi wake walizuiliwa kufuatilia hesabu ya kura, ikibainisha kuwa uwazi ulibanwa.
Ripoti iliongeza kusema katika baadhi ya vituo vya kupigia kura waangalizi waliruhusiwa kuangalia upigaji kura kwa dakika tano pekee.
Umoja wa Afrika umeitaka Tanzania kuyapa kipaumbele mageuzi ya sheria za uchaguzi na kisiasa ili kushughulikia sababu kuu za changamoto zake za kidemokrasia na uchaguzi.
Chanzo; Dw