Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amesema Kilimanjaro Native Cooperative Union (KNCU) imeanza kulipa fedha zinazodaiwa na vyama vya msingi vya ushirika kufuatia agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni.
Amesema hatua hiyo inalenga kumaliza malalamiko ya muda mrefu ya wakulima wa kahawa waliokuwa wakisubiri malipo yao baada ya kuuza mazao kupitia chama hicho kikuu cha ushirika.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kuhusu makadirio ya mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Mkuu huyo wa Mkoa amesema vyama 12 vya msingi vilikuwa vinadai jumla ya shilingi milioni 412.
Ameeleza kuwa vyama vinane tayari vimepokea fedha zao, ambazo zimeingizwa moja kwa moja katika akaunti zao, huku vyama vilivyosalia vikitarajiwa kulipwa ifikapo Machi 6 mwaka huu.
Kwa mujibu wake, changamoto hiyo ilichangiwa na kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia wakati KNCU tayari ilikuwa imepokea mazao ya wakulima. Kutokana na hali hiyo, chama hicho kililazimika kukopa katika Benki ya Ushirika ili kuanza kulipa madeni.
Akizungumza na Nipashe, mmoja wa wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Mwika Kinyamvuo, Glory Sam, amesema tayari wakulima wa chama chao wamepokea fedha zote walizokuwa wakizidai, jambo lililopunguza wasiwasi uliokuwepo kwa muda mrefu.
Awali, Waziri Mkuu akiwa katika ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Kilimanjaro Februari 20 mwaka huu, alilitaka KNCU kuuza baadhi ya mali zake ili kulipa deni la zaidi ya shilingi milioni 412 lililokuwa likidaiwa na wanachama.
Canzo; Nipashe