Jeshi la Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya limethibitisha kifo cha Dafroza Kokwangua Jacob, maarufu kama Mama Frank, kilichotokea jana Jumatano, Novemba 5, 2025, majira ya saa 1:00 jioni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo, Mama Frank alizidiwa ghafla akiwa katika mahojiano na maafisa wa polisi kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Taarifa inazidi kueleza kuwa baada ya kupata hali mbaya, alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini akiwa anaendelea kupatiwa huduma za kitabibu, alifariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya amesema uchunguzi wa kina umeanza mara moja kwa kushirikiana na wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi (forensic experts) ili kubaini chanzo kamili cha kifo hicho.
Aidha, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa taarifa zaidi zitatolewa mara baada ya uchunguzi kukamilika, na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati taratibu za kijinai na kitabibu zikiendelea.
Chanzo; Global Publishers