Watoto wawili wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiembeni Bagamoyo waliopotea Desemba 30, 2025, wamepatikana jijini Dar es Salaam kufuatia juhudi za Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wananchi ambapo walikutwa wakiishi nyumbani kwa mjumbe wa Serikali za Mitaa wa Mwenge jijini humo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema mjumbe huyo alieleza kuwa watoto hao, Rachel Zacharia na Joseph Zacharia (wote miaka 12), walipelekwa kwake na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo baada ya kuwakuta katika kituo cha daladala cha Mwenge wakiishi maisha ya mitaani.
RPC Morcase amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa watoto hao waliondoka nyumbani kwao Mapinga, wilayani Bagamoyo, wakikimbia adhabu walizokuwa wakipewa shuleni na nyumbani kutokana na utoro, pamoja na manyanyaso kutoka kwa dada waliokuwa wanaishi naye.
“Huko Bagamoyo walikua wanaishi na Dada Yao ambaye ni Askari wa JWTZ lakini sass tayari tumewachukua watoto hao na kuwapeleka katika nyumba salama kwa uangalizi maalum kabla ya kukabidhiwa kwa baba yao anayeishi Musoma. " Amesema na kuongeza
Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kutambua kuwa watoto wana haki ya kulindwa na kulelewa katika mazingira salama,” amesema RPC Morcase.
Katika tukio jingine, Agnes Liku (35), mkazi wa Msimbi wilayani Kisarawe, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa amejifungua mtoto katika zahanati ya Kijiji cha Mwanzomgumu, kisha kudai mtoto huyo alichukuliwa na Afisa Tabibu asiyejulikana.
Chanzo; Wasafi